Msichana wa miaka 14 jina limehifadhiwa,anashikiliwa na
jeshi la polisi mkoani Pwani kwa tuhuma ya kumuua mtoto wake Mariam Stamili
mwenye miezi tisa kwa kisingizio cha ugumu wa maisha.
Kamanda wa Polisi Pwani Ulich Matei amedhibitisha tukio ambapo amesema
limetokea huko Mlandizi Kibaha na kwamba mama huyo anadaiwa kumuua mtoto wake
huyo baada ya kumnywesha sumu inayodhaniwa ni ya kuulia panya.
Amesema mama huyo alifikia uamuzi wa kumnywesha sumu ya panya mtoto huyo akiwa
nyumbani kwake Mlandizi na muda mfupi alipoona hali ya kichanga hicho inakua
mbaya alimpigia simu mzazi mwenzake baba wa mtoto Stamili Shaban (21)na
kumueleza kuwa anaumwa sana.
Baba mtoto alifika kumjulia hali mwanaye na kweli alimkuta ana hali mbaya na
mke wake kumueleza kuwa kichanga hicho kinasumbuliwa dege dege hivyo walikubaliana
kwenda kumtafutia matibabu.
Hata hivyo wazazi hao walimpeleka kwa mganga wa kienyeji huko Kijiji cha
Disunyara ambapo marehemu alianza kupatiwa matibabu lakini hali yake ilizidi
kuwa mbaya na kulazimika kumuhamishia kituo cha afya Mlandizi ambapo
alifariki dunia kabla hata ya kuanza tiba.
Matei ameongeza kuwa uchunguzi wa awali katika kituo cha afya hicho umebaini
kuwa chanzo cha kifo hicho ni kunyweshwa sumu inayosadikiwa kuwa ni ya
panya .
Amebainisha kuwa uchunguzi zaidi umebaini siku ya tukio mtoto huyo hakuwa na
ugonjwa wowote bali mama yake aliamua kununua sumu hiyo na kumnyweshwa na hali
ilipobadilika alimpigia simu mume wake na kumueleza mtoto wao
anasumbuliwa na degedege .
Mwili wa marehemu umechukuliwa na ndugu
na kuzikwa huko Kijiji cha Kilangalanga,
huku majirani wakishuhudia mama huyo akilia na kusema chanzo cha kifo ni yeye
mwenyewe na si degedege kama alivyosema awali,hivyo asamehewe.
Matei amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma dhidi yake baada
ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment