WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka maafisa mipango miji nchini kurekebisha
utendaji wao wa kazi ili waweze kubadili taswira mbaya iliyojengeka
miongoni mwa jamii dhidi yao.
Ametoa
kauli hiyo huo leo mchana (Alhamisi, Novemba 27, 2013) wakati akifungua
Mkutano wa Kwanza wa Wataalam wa Mipangomiji waliosajiliwa na Bodi ya
Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji ulioanza leo jijini Dar es Salaam.
“Taswira
ya utendaji kazi katika taaluma ya mipangomiji na katika sekta ya
ardhi kwa ujumla miongoni mwa wananchi na Serikali siyo nzuri sana.
Watafiti wanatueleza kuwa kati ya asilimia 60 na 80 ya makazi kwenye
miji yetu hapa nchini yamejengwa kiholela. Na kwa kiwango hicho hicho
wakazi wa mijini wako kwenye makazi hayo na wanaishi kiholela,” alisema.
“Wako
wanaosema ninyi ndiyo chanzo cha hiyo migogoro, wako wanaosema ninyi kwa
rushwa ndiyo wenyewe, mimi sishangai madai haya ila ninawasihi muwe na
roho ngumu katika kushinda vishawishi hivi,” alisisitiza.

Aliwataka
wajadili masuala yanayohusu migogoro ya ardhi bainaya wafugaji na
wakulima, baina ya mipaka ya vijiji, baina ya wilaya, baina ya
wanavijiji na hifadhi za Taifa au maeneo ya uchumbaji madini na kujadili
njia za kutatua migogoro hiyo ili kuwa na mipamgo endelevu.
Aliwataka
waangalie suala la ukuaji wa miji iliyokaribu na Jiji la Dar es Salaam
kwa kuangalia dhana ya miji mikubwa kubeba vijiji vinavyoizunguka na
hasa kuangalia uwezekano wa kupunguza mlundikano wa watu katika jiji
hilo. “Miji ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo inatumikaje kusaidia
kupunguza msongamnano katika jiji la Dar es Salaam,” Waziri Mkuu alihoji
Alisema
wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuwa na maono makubwa ya baadaye
kama kweli wanataka kupunguza majanga katika siku za usoni. “Angalieni
utafiti wa gesi unaoendelea pale Mtwara na mjipange, angalieni mpango wa
ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na kuunganisha na reli ya kati, angalieni
Lindi na upatikanaji wa Liquified Naturala Gas (LNG), pangeni miji kwa
siku za baadaye siyo sasa,” alisisitiza.
Aliwataka
wanataaluma hao wasimamie vema taaluma yao kwani katika miaka 37 ijayo,
(mwaka 2050) inakadiriwa kwamba nusu ya watu wote watakuwa wakiishi
mijini. “Kuweni wakweli, tumieni weledi wenu la sivyo katika miaka 37
ijayo kama wanavyosema watafiti, itakuwa balaa tupu,” alisema.
Mapema
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wataalamu hao kutoka mikoa yote
hapa nchini, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna
Tibaijuka alisema maafisa mipango miji wanakabiliwa na changamoto ya
kufikiri na kubuni aina ya miji ambayo itakidhi mahitaji ya jamii ya
baadaye.
Alisema
hata hivyo maafisa hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kushindwa
kutoa maamuzi ama ushauri wa kitaalamu kwa kuhofia kuadhibiwa na
madiwani.
Mkutano
huo wa siku mbili unafanyika katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo na
unatarajiwa kufungwa kesho na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
No comments:
Post a Comment