Jahazi hilo lilikamatwa jana saa sita usiku kwenye Bahari ya Hindi, mwambao wa Bandari ya Dar es Salaam na askari wa doria wana-maji wakishirikiana na kikosi cha kupambana na kudhibiti dawa za kulevya nchini.
Jahazi hilo likiwa na dawa hizo zinazodhaniwa kuwa ni heron kilo 201, limeshikiliwa pamoja na raia wa Pakistan na Iran wapatao 12 ambao walikuwa ndani ya jahazi hilo.
Gazeti la Majira lilishuhudia kikosi cha kupambana na dawa za kulevya na wanamaji wakifanya upekuzi katika jahazi hilo kwa muda mrefu bila kubaini ni wapi zilikuwa zimefichwa.
Jahazi hilo lilifanyiwa upekuzi wa kutosha kwa kusaidiana na Wakufunzi wa Polisi kutoka Marekani ambao wapo nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa Polisi Wanamaji jinsi ya kunasa dawa za kulevya.
Wataalamu hao waliobobea kwenye eneo hilo, waliifanyia utafiti wa kina jahazi hilo kwa muda mrefu huku wafanyakazi wa jahazi hilo wakikataa katakata kwamba hakuna dawa hizo.
"Ilifika wakati wakataka kuachiwa maana hakukuwa na dalili za kuwepo dawa hizo wala chochote cha hatari huku wakilalamikia waliokuwa wamewakamata kwa hoja kwamba wanawapotezea muda, kwani wao wapo kwenye harakati za uvuvi," kilisema chanzo na kuongeza;
"Tulitaka kuwaachia, lakini wenzetu wa Marekani kutokana na utaalamu walionao walikataa kuwaachia kirahisi na kufanya upekuzi zaidi, ambapo kati ya sehemu tatu kwenye meli hiyo, walilazimisha sehemu moja itobolewe ili kuingia ndani zaidi ambako ndiko kulikobainika kuwepo chumba chenye shehena ya dawa hizo."
Akizungumza baada ya kupakua shehena hiyo ya dawa, Kamishna Polisi Msaidizi na kamanda wa Kikosi cha Wanamaji, Mboje Kanga, alisema kikosi chake kwa kushirikiana na kikosi cha dawa za kulevya walibaini jahazi hilo lilitoka Iran jana usiku saa sita.
Alisema baada ya kutilia shaka kutokana na uchakavu wake, walihitaji kulifanyia upekuzi ili kujua lina nini. Alisema thamani halisi ya dawa hizo haijajulikana wala mtandao uliokuwa ukitarajiwa kupokea mzigo huo nchini.
Alisema watuhumiwa hao wamegoma kuzungumza lugha yoyote zaidi ya Kipakistani na Kiarabu, hivyo upelelezi zaidi unaendelea.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti Dawa ya Kulevya, Godfrey Nzoa, alisema dawa hizo zinadhaniwa kuwa ni Heron. Alisema kukamatwa kwake ni mwendelezo wa mkakati wa kupambana na vitendo haramu vya madawa ya kulevya.
Alisema kwa kushirikiana na watu wa Interpool wamekuwa na mafanikio makubwa kupata wahalifu wa matukio hayo kutoka nchi mbalimbali ambapo katika tukio hilo wamebaini jahazi lililobeba mzigo huo linaitwa Aldanial ambalo limetoka nchini Iran.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Charles Tizeba, akizungumzia kukamatwa kwa jahazi hilo eneo la tukio, alisema huu ni wakati mwafaka mataifa yanayodhani kuwa Tanzania ni uchochoro wa biashara haramu ya dawa za kulevya kufuta dhana hiyo, kwani hatua zaidi zitachukuliwa kukabiliana na wote wanaohusika katika matukio hayo ili kujenga heshima ya nchi.
Alisema mbali na kukamata watuhumiwa hao wataendelea kuwatangaza kwenye vyombo vya habari na vyombo vya sheria kuchukua hatua zaidi, kwani hakuna atakayeachwa katika vita hii.
“Tanzania si uchochoro wa biashara hii haramu na tutahakikisha tunawachukulia hatua kweli kweli hasa hawa jamaa na kama ningekuwa ni mimi natoa hukumu ningechukua uamuzi mgumu, kwani wao wanaua maelfu ya vijana wetu; ni watu hatari sana mzigo mkubwa kama huu ni vijana wangapi nguvukazi ya Taifa hili wangekuwa mazezeta au hata kubebeshwa kupeleka nchi nyingine... inasikitisha sana," alisema.
Aliwataka wabunge wenzake sasa kuona umuhimu wa tatizo hilo kwa nchi, kwani adhabu haitoshi na wakati umefika wa kutunga sheria kali ambayo itawafanya watu hawa kujuta na kutokurudia kuchezea nchii hii.
Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na nahodha wa Jahazi, Ayoub Hot (50) raia wa Iran, Abdulsamad Badreuse (47) Iran,Muhamad Hasan (30) Pakistani, Hazra Azat (60) Iran, Nahim Musa(25) Iran, Khalid Ali (35) Iran, Abdul Nabii (30) Pakistan, Rahim Baksh(30) Pakistan, Kher Mohamed (75) Iran, Said Mohamed (34) Iran, Murad (38) Iran na Fahiz Mohamed (34), Pakistan.
Chanzo;Majira
No comments:
Post a Comment