Awachoma moto mikononi kwa tambi za jiko


Watoto wanaodaiwa kufanyiwa ukatili wakionyesha
vidonda kwenye mikono yao ambavyo vinatokana na kuchomwa moto na baba ya
mzazi nyumbani kwao Mbagala Kibondemaji jijini Dar es Salaam jana.
Picha/ Omar Fungo
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanywa na
baadhi ya wazazi, vimezidi kukithiri nchini baada ya watoto wawili
kudaiwa kuchomwa moto mikono na baba yao kwa kutumia tambi za jiko
jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, anayetuhumiwa kufanya unyama
huo ni Salum Juma, fundi gereji wilayani Temeke, mkazi wa Mbagala
Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam.
Watoto hao mmoja mwenye umri miaka saba na mwingine miaka mitano (majina
yao yamehifadhiwa), akiwamo wa kumzaa na wa kufikia walikutwa na mkasa
huo baada ya kwenda kuangalia runinga kwa jirani na kurudi nyumbani saa
5:00 usiku Alhamisi wiki iliyopita.
Akizungumza na NIPASHE, jirani yao, Omar Fusi, alidai watoto hao
walieleza kuwa walichomwa na baba yao na kufichwa ndani, lakini baadaye
majirani waliwaona watoto hao wakiwa na majeraha.
Fusi alisema baada ya kuwaona wakiwa na majeraha, waliwahoji ambapo
walieleza kuwa walichomwa na baba yao baada ya kuchelewa kurudi kutoka
kuangalia televisheni.
Kwa mujibu wa Fusi, kitendo hicho kilifanyika huku mama yao akiwa kwenye biashara zake za kukaanga mihogo.
Fusi alisema baada ya kubaini tukio hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Kibonde Maji ‘B’, Teofile Balae, ambaye alitoa
taarifa kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kata ya Mbagala, Eliameresa Kaaya na
kuripoti polisi na kufanikisha baba huyo kukamatwa na kupelekwa katika
Kituo cha Polisi Maturubai ambako anaendelea kushikiliwa.
Balae alisema baada ya kushirikiana na Ofisa Ustawi wa Jamii na baba
huyo kukamatwa, waliwachukua watoto hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi
Mbagala Kuu kwa ajili ya kupata fomu ya PF3 na kuwapeleka katika
hospitali ya Mbagala Rangi Tatu kupatiwa matibabu.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Erasto Kibara, alisema walibaini watoto
hao kufanyiwa ukatili huo baada ya kumkuta mmoja wao adukani alikotumwa
akiwa na majeraha na kumuuliza kilichompata kisha alitoa taarifa hizo
kwa mwenyekiti wa mtaa huo.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Kaaya, akizungumza na NIPASHE katika Kituo cha
Polisi Maturubai wakati watoto hao wakichukuliwa maelezo na polisi,
alisema kitendo walichofanyiwa watoto hao ni cha kikatili na kuwataka
wananchi kutoa taarifa pale wanapogundua ukatili katika mitaa yao ili
kutokomeza vitendo hivyo vilivyoshika kasi nchini.
NIPASHE iliwashuhudia watoto hao katika Kituo cha Polisi Maturubai huku
wakiwa na majeraha mkononi wakati wakichukuliwa maelezo na maofisa wa
polisi wa kituo hicho.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dk. Julius
Nyakazilibe, alithibitisha watoto hao kupokelewa hospitalini hapo na
kupatiwa huduma ya matibabu kutokana na majeraha yaliyosababishwa na
moto.
“Ni kweli watoto hao tuliwapokea hapa hospitalini wakiwa na Ofisa Ustawi
wa Jamii na walipatiwa matibabu,” alisema Dk. Nyakazilibe. Mama mzazi
wa watoto hao, Christina Menasi, akiwa katika kituo cha polisi na mtoto
wake mchanga huku akimnywesha uji, alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa
katika biashara yake ya kuchoma mihogo na aliporudi nyumbani na kukuta
hali hiyo, aliingiwa na hofu ya kuripoti tukio hilo kwa kumhofia mumewe.
Mama huyo alilaani kitendo hicho cha kikatili lakini alisema akifungwa yeye ndiye atakuwa na mzigo mkubwa wa kulea familia hiyo.
“Inatakiwa tuache vitendo hivi vya kikatili, lakini ikiwa mume wangu
atafungwa, mimi ndiye nitakayebeba mzigo wa kulea hii familia,” alisema
Christina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha
Polisi Maturubai na kwamba upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa
mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment