Mafundi wakiendelea na kazi za ujenzi wa daraja kubwa la Kolo lenye urefu wa mita 60 katika barabara ya Dodoma-Babati sehemu ya kipande cha barabara ya kutoka Mela kwenda Bonga chenye urefu wa km 88.8. Ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu (watatu kutoka kushoto) akiwa na wahandisi wa barabara ya kutoka Mela-Bonga mara baada ya ukaguzi wa daraja la Kolo.
Mafundi wakisuka nondo kwa ajili ya kumalizia kalavati la duara katika barabara ya Dodoma (Mayamaya) hadi Babati (Bonga) katika sehemu ya Mela kwenda Bonga km 88.8.
Mhandisi mshauri katika barabara ya Mayamaya-Mela km 99.35 Eng. Godfrey Kombe akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi wa barabara hiyo uliofikia asilimia 18.
Kazi za ujenzi zikiendelea kwenye tuta la barabara ya Mayamaya-Mela km 99.35.
Kazi za ujenzi zikiendelea kwenye tuta la barabara ya Mayamaya-Mela km 99.35.
Fundi akichomelea vyuma katika sehemu litakapojengwa boksi kalavati.
Katapila likichonga barabara ya Mayamaya-Mela km 99.35.
Boksi kalavati likiwa limekamilika katika
barabara ya Mayamaya-Mela km 99.35.(Picha zote kwa Hisani ya Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini (GCU)-Wizara ya Ujenzi)
Ujenzi wa Barabara ya Dodoma (Mayamaya) hadi
Babati km 188.15 katika sehemu ya Mayamaya-Mela km
99.35 pamoja na kipande cha Mela Bonga km 88.8 unaendelea vizuri na
unatarajiwa kukamilika mwaka 2017.
Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa Wakala wa
Barabara Mkoani Dodoma Eng. Leonard Chimagu wakati akifanya ukaguzi wa ujenzi
wa barabara hiyo inayojulikana kama barabara kuu ya
Kaskazini iliyoanzia Cape town nchini Afrika Kusini hadi Cairo
nchini Misri
“Katika barabara kuu hiyo sehemu yetu ya
Tanzania ndio ilikua haina lami ila kwasasa ujenzi umeanza na unaendelea
vizuri, ujenzi wa barabara katika sehemu ya kwanza ya Mayamaya-Mela km
99.35 umefikia asilimia 18 na ule wa Mela Bonga km 88.8 umefikia
asilimia 20 ya ujenzi wake” alisema Eng. Chimagu.
Eng. Chimagu aliongeza kuwa mkandarasi
yupo katika hatua za mwanzo na anaendelea vizuri na kama hakutakuwa
na vikwazo vyovyote basi ataikamilisha barabara hiyo kwa wakati”, alisema Eng.
Chimagu.
Kwa upande wa Mhandisi Mshauri katika sehemu
ya barabara ya Mayamaya-Mela km 99.35 Eng. Godfrey Kombe
alisema kuwa kazi za ujenzi zinaendelea vizuri na tayari mkandarasi
ameshasafisha eneo la barabara lenye urefu wa km 70.
“Tayari Mkandarasi ameshasafisha eneo la
barabara lenye urefu wa km 70 kwa kuondoa miti mikubwa, pia ameweza kujenga jumla
ya makalavati 52 ya duara pamoja na 12 ya boksi”, alibainisha Eng. Kombe.
Aidha, Eng. Kombe amesema kuwa ujenzi huo
unahusisha pia ujenzi wa madaraja makubwa manne moja likiwa na urefu wa mita
200 na mengine yakiwa na urefu wa mita 45 pamoja na mita 30 madaraja mawili.
Kwa upande wa ujenzi wa sehemu ya barabara ya
Mela-Bonga km 88.8 Eng. Chimagu amesema kuwa unaendelea vizuri na ujenzi wa
daraja kubwa la Kolo lenye urefu wa mita 60 unatarajiwa kukamilika mwezi
mei mwaka huu.
Aidha, Mhandisi Mshauri wa kipande hicho cha
barabara ya Mela-Bonga- km 88.8, Eng. Kini Kuyonza alisema kuwa mkandarasi
wa barabara hiyo amefikia hatua nzuri kwa asilimia 20 na ujenzi unaendelea kama
walivyopanga.
Mradi huo wa ujenzi wa Barabara ya Dodoma
(Mayamaya) hadi Babati (Bonga) yenye urefu wa Km 188.15 unagharimu kiasi cha
zaidi ya shilingi bilioni 183.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini (GCU)-Wizara ya Ujenzi
No comments:
Post a Comment