
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto
la Mbeya baada ya meya wa jiji
hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34 kususia kikao chake cha
kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa
bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji hilo.
Meya alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda
mfupi kabla ya Makalla kuanza kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi, wazee
maarufu, viongozi wa dini na machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyirembe
Sabi alimkaribisha Meya Mwashilindi kuzungumza chochote kwa niaba ya madiwani
wake.
Hata hivyo, Meya Mwashilindi alipochukua kipaza sauti
alisema: “Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, nakumbuka kwa mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba
tufanye kazi, siasa zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii
umekwenda Soko la Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala
madiwani wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”
Baada ya kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti
kwa mkuu wa wilaya, kisha
akachukua nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia Chadema na
kutoka ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi
ni siasa ambazo tulizikataa, lakini wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi
kupuuzwa kwa kiasi hiki.”
Mkuu wa Wilaya, Mnasa alisema anaamini taratibu na
ratiba yote ilipangwa vizuri hivyo hawaoni sababu ya madai ya madiwani hao
kwamba hawakushirikishwa kwenye ziara hiyo, wao kama wawakilishi wa Rais
hawaangalii siasa, bali wanaangalia uchapakazi na siyo masuala ya siasa.
Akizungumzia kitendo cha meya na madiwani wake kususia
kikao hicho, Makalla alisema ‘Nashangazwa na uamuzi wa madiwani hawa kwa
kitendo hiki, kwani siku ile nilipotembelea Shule ya Sekondari Iyunga, nilisema
kwamba Aprili 20 ambayo ndiyo leo (jana) nitakuwa na ziara ya jiji na kabla ya
kikao nitataka kutembelea Soko la Mwanjelwa,” alisema Makalla.
Alisema suala la meya na madiwani wake kutoshirikishwa
kwenye ziara ya kwenda Soko la Mwanjelwa halimhusu, kwani mwenye wajibu wa
kupeana taarifa ni kwenye ngazi ya halmashauri ya jiji, lakini siyo yeye
(Makalla).
“Jamani mimi sijaja kufanya siasa nimekuja kufanya
kazi ya wananchi na nilishatahadharisha jambo hili, sasa kwa kitendo hiki ndiyo
siasa na wananilazimisha kufanya siasa, lakini wao ndiyo watahukumiwa na
wananchi. Na ninasema kama Mola ataendelea kunilinda kubaki katika mkoa mwaka
2020 nitakwenda kuwaambia hiki kinachofanyika sasa na wawakilishi wao,” alisema Makalla.
Awali Makalla akiwa katika Soko la Mwanjelwa alinusa
harufu ya ufisadi kwenye soko hilo na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoa
huo, kufanya uchunguzi ndani ya wiki nne wa uhalali wa fedha kiasi cha Sh22.9
bilioni iliyotumika katika ujenzi huo ukiwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Makalla alitoa agizo hilo jana mchana baada ya
kutembelea soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara wa jijini hapa, ambao
walimueleza wanashindwa kumudu gharama ya upangaji ya vyumba vya biashara
ambayo inaanzia kiasi cha Sh500,000 kwa chumba kimoja kwa mwezi, ndiyo maana
hawataki kuingia ndani ya soko hilo.
Mwenyekiti wa soko hilo, Peter Chacha alimueleza
Makalla kwamba wasipokuwa makini soko hilo litabaki gofu, kwani wafanyabiashara
hawataki kuingia kwa kuogopa gharama kubwa ya vyumba hivyo, alimuomba afanye
awezalo kukaa chini na uongozi wa benki ambao unadai fedha zao kwa jiji na
kuona namna ya kupunguziwa gharama hiyo.
“Ni kweli wenzetu
jiji, wametingwa na deni la mkopo kutoka Benki ya CRDB, ndiyo maana wamekuja
kutubana sisi wafanyabiashara kwa kutupangia chumba kuanzia Sh500, 000 hadi Sh
800,000, kitu ambacho hatuwezi kumudu hata kidogo,”alisema Chacha .
Baada ya kusikiliza kilio cha wafanyabiashara hao,
Makalla alisema kiasi cha Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi wa soko hilo
haiendani na thamani yake, hivyo vyombo vya dola vikiongozwa na Kamanda wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, wanafanya
uchunguzi wa kina na kuwanasaka wale wote waliohusika kwenye mchakato mzima wa
ujenzi wa soko hilo.
“Nataka kupata taarifa ya mchanganuo mzima wa namna ya
fedha ilivyokopwa, ilivyotumika na mkataba wake ulivyokuwa ndani ya wiki nne,
taarifa hii niipokee na wale watakaobainisha kufuja fedha watapelekwa
mahakamani kwa mujibu wa sheria.
"Kwenye hili, kuna watu waliotufikisha hapa,
Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi huu haiendani na ujenzi wa soko hili,
kuanzia muda uliotumika na gharama ya kodi ya upangishaji wa vyumba siyo rafiki
ni kubwa mno, hivyo jiji na CRDB mkae muone namna ya kupunguza gharama hiyo,
kwani hali ilivyo sasa lile soko litabaki gofu."
No comments:
Post a Comment