
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Leonard Swai ameiomba mahakama iingilie kati kile alichokiita
rushwa ya kutisha kwenye taasisi hiyo ya kutoa haki.
Wakili Swai alitoa wito huo baada ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuachia huru mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco), William Geofrey Mhando na wenzake wanne akiwamo mkewe
Eva Mhando, katika kesi aliyokuwa akiiendesha.
Katika kesi hiyo, Mhando, mkewe na maofisa wengine
watatu wa zamani wa Tanesco;
France Lucas Mchalange, Sophia Athanas Misida na Naftali Luhwano Kisinga,
walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na
kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali.
Hata hivyo, washtakiwa hao wameibwaga Takukuru baada
ya mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi
yao.
“Haki haijatendeka na tunatarajia kukata rufaa,” alisema Wakili Swai alipozungumza na waandishi nje ya mahakama.
“Rushwa iliyopo mahakamani inatisha. Serikali
inatakiwa kuingilia kati.”
Hata hivyo, wakili huyo hakueleza rushwa hiyo
ilifanyikaje katika kesi hiyo ambayo iliendeshwa na taasisi hiyo iliyopewa
dhamana ya kuzuia na kupambana na jinai hiyo.
Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Aprili Mosi mwaka
huu na Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema aliyekuwa akisiliza kesi hiyo, lakini
ikaahirishwa hadi Aprili 6, ambayo pia ilisogezwa mbele hadi jana iliposomwa na
Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Rusema, Hakimu
Riwa alisema kwa mujibu wa ushahidi, suala la msingi lilikuwa ni mkataba kati
ya kampuni ya Santa Clara Supply Limited na Tanesco.
Alisema katika mkataba, Mhando, ambaye alikuwa
mshtakiwa wa kwanza, alituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa
kutangaza maslahi yake kuwa kampuni ya Santa Clara ni ya Eva Mhando ambaye ni
mkewe.
“Suala la msingi la kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo
anahusika katika utoaji wa zabuni na nani aliyekuwa na maamuzi ya mwisho,” alisema Hakimu Riwa akisoma hukumu hiyo iliyoandaliwa
na Hakimu Rusema.
“Jibu la swali hilo ni kwamba Bodi ya Zabuni ya
Tanesco ndiyo iliyohusika na mchakato huo.”
Hakimu Riwa aliongeza kuwa miongoni mwa washtakiwa
hao, hakuna hata mmoja aliyekuwa mjumbe katika vikao vilivyoendeshwa na bodi
hiyo ya zabuni, wala kuitwa kuhudhuria mkutano wowote wa bodi hiyo.
“Kutokana na sababu hiyo, inawezekana vipi mshtakiwa
huyu akatangaza maslahi yake katika mkutano ambao hakuhudhuria?”
Kuhusu suala la mshtakiwa huyo kujua kama Santa Clara
inamilikiwa na mkewe na watoto wake, alisema kuwa inawezekana asijue kama wana
kampuni.
Alisema kuwa hakuna ushahidi kuwa mshtakiwa huyo
aliulizwa swali lolote kuhusu kampuni hiyo.
Katika kusisitiza hoja hiyo, Hakimu Rusema katika
hukumu yake hiyo alitoa mfano kuwa mwanamke anaweza kufungua akaunti kwa siri
benki na akaweka fedha kisha mumewe asijue.
Kuhusu suala la mshtakiwa wa pili, Eva, kughushi
nyaraka na kuziwasilisha Tanesco, alisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha
kuwa alifanya kosa hilo na kwamba aliyesaini nyaraka hizo ni mtu mwingine
ambaye hata hivyo hakushtakiwa.
Wakati wote Hakimu Riwa alipokuwa akisoma hukumu hiyo,
baadhi ya watu ambao wanasadikiwa kuwa ndugu wa washtakiwa hao, walionekana
wakifanya ishara ambazo zilionyesha wanamuomba Mungu.
Baada ya hukumu hiyo na kuachiwa huru, Mhando
alionekana kutoamini na alipotoka mahakamani, alielekea moja kwa moja kwenye
gari lake na kukataa kuongea na mtu yeyote.
Hali hiyo ilionekana kuwatia hofu ndugu zake ambao
baadhi walimshauri asiendeshe gari, badala yake aendeshwe kwa kuhofia kuwa kwa
hali aliyokuwa nayo angeweza kusababisha ajali.
“Msimuachie aendeshe, Mhando kaa kiti cha nyuma,” alisema mmoja wa ndugu zake. Mhando alikubali na
kuhamia kiti cha nyuma kisha mkewe naye aliingia kwenye gari hilo na kuondoka
viwanja vya mahakama.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya
kwanza Mei 26, 2014 na kusomewa mashtaka na Wakili Swai.
No comments:
Post a Comment