Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, Edward Lowasa amemtaka Rais John Magufuli kuwa na utamaduni wa kufanya
mazungumzo na wanasiasa wenzake ili kufikia muafaka wa mambo mbali mbali ya
kisiasa nchini.
Lowasa ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na Tido
Mhando kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na Televisheni ya Azam.
Lowasa amesema kuwa siasa ni mazungumzo na siyo kutoa tu amri kama anavyofanya
Rais Magufuli.
Kadhalika Lowassa amesema kila mtu ana wajibu wa
kuheshimu amani ya nchi na hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi hii.
“Serikali haipaswi kuwa na
ghadhabu, inapaswa kuwa na tabia ya kuzungumza. Sisi sote ni Watanzania kwa
nini tunaogopa kuzungumza. Mazungumzo ndiyo njia bora ya kufikia maridhiano.
Pia Rais Magufuli aitazame Zanzibar, tunasikia watu wanashughulikiwa kwa njia
mbalimbali, wanakamatwa, hivyo hawezi kuikwepa Zanzibar kwani hilo ni suala
lake.” alisema Lowassa.
Amesema CHADEMA ipo sahihi kutangaza operesheni
‘Ukuta’ hapo Septemba 1, mwaka huu na kwamba bado kuna nafasi ya kufanya
mazungumzo kabla ya tarehe hiyo kufika ili kuepusha hali ya migogoro
itakayojitokeza siku hiyo itakapofika.
Akizungumzia barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa
kukemea operesheni hiyo, amesema barua hiyo imejaa ghadhabu zaidi kuliko
kuongelea mambo ya msingi ambayo vyama vya upinzani vimekuwa vikionewa.
Akiongelea suala la wabunge wa upinzani kutoka na
kususia bunge, Lowassa amesema hali hiyo ilisababishwa na kutokuwepo kwa Spika
Job Ndugai ambaye kwa muda mrefu alikuwa nje ya nchi akiendelea na matibabu.
“Ndugai angekuwepo haya
yote yasingetokea kwakuwa ni mtu makini sana na hata kwa Naibu Spika kuna
tatizo la Kisaikolojia kwasababu aliingia bungeni kwa njia zisizoeleweka na
hivyo kumfanya kushindwa kuhimili kiti vizuri,” amesema.
Hata hivyo amempongeza Rais Magufuli na kudai kuwa
amefanya vizuri katika baadhi ya maeneo lakini kuna maeneo mengine ambayo
angepaswa kuyapa kipaumbele zaidi akitolea mfano wa elimu na kudai kuwa badala
ya kuanza na suala la madawati angeanza na kushughulikia maslahi ya walimu
kwanza, na kutoa kipaumbele kwa tatizo la ajira nchini hasa kwa vijana.
Kuhusiana na harakati za Serikali kuhamia Dodoma,
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu CHADEMA amesema viongozi wote waliotangulia tangu
enzi za Mwalimu Nyerere walikuwa na ndoto za kuhamia Dodoma lakini kuna mambo
yaliyokuwa yanaingilia mipango hiyo na mwisho kushindikana.
“Napongeza harakati na
dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia Serikali yote Dodoma lakini
napenda kuwaambia wasiende kwa kasi sana wasije wakavunjika miguu,” ameongeza.
Kuhusiana na hali ya kisiasa Zanzibar, Lowassa ametoa
rai kwa Rais Magufuli aangalie hali ya Zanzibar kwani yanayoripotiwa kuendelea
visiwani humo yanatia kichefuchefu ikiwemo watu kukamatwa na kuteswa.
“Tusiitenge Zanzibar na
badala yake juhudi za makusudi zifanyike kuweka mambo sawa kwa kufanya
mazungumzo kwani siasa ni mazungumzo,” amesisitiza Lowassa ambaye amedai kuwa ana matumaini
makubwa ya kuingia Ikulu mwaka 2020.
Kuhusu kashfa ya Richmond kumfanya aondoke CCM kwa
hasira baada ya kukosa ridhaa ya chama hicho katika kugombea Urais, Lowassa
amesema hakuondoka CCM kwa hasira isipokuwa alituhumiwa na kuhukumiwa bila
kupewa nafasi ya kusikilizwa.
“CHADEMA sikujipeleka
mwenyewe bali Kamati Kuu CHADEMA ilinifata na kuniomba nijiunge nao katika
kupeperusha bendera yao na mimi niliona ni ‘opportunity’ nzuri hivyo nikakubali
nikajiunga nao na tukafanikiwa kupata kura zaidi ya milioni sita, idadi ambayo
siyo ndogo hata kidogo,” amejinasibu Lowassa.
No comments:
Post a Comment