
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaotumia vibaya madaraka, wakiwamo wanaojihushisha na vitendo vya rushwa.
Pia amesema serikali inafanya mapitio ya sera, sheria na kanuni ili kuendana na mbadiliko ya wakati, ikiwamo kuanzisha Mahakama ya Mafisadi.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana bungeni, mjini hapa, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa.
Mbunge huyo alihoji kama sera na mifumo ya kisheria iliyopo sasa inaruhusu kuwa enzi waasisi na viongozi wa nchi lakini siku za hivi karibu kumekuwapo na baadhi ya viongozi kujihusisha na wizi, ubadhirifu wa mali za umma na ukiukwaji wa maadili.
“Je lini serikali itafanya mapitio ya sera, sheria na kubadilisha mifumo ili sasa wale wezi wote waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria?” alihoji.
Majaliwa alisema serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watumishi kufuata maadili ya utumishi, ikiwamo uadilifu, uaminifu na uchapakazi.
“Tunaendelea kuboresha kwa kuunda taasisi ya maadili kwa watumishi wa umma ambayo yenyewe inajiridhisha kila mtumishi anatangaza mali zake na kuendelea kufuatilia mara kwa mara mabadiliko ya mali hizo ili kuona imepatikana kihalali,”alisema Majaliwa
Pia alisema serikali inaendelea kuimarisha taasisi mbalimbali, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambayo inafuatilia maeneo yote kwa watumishi wa umma na raia wa kawaida.
“Ili kudhibiti tabia hii, sasa serikali kupitia Bunge hili waheshimiwa wabunge siku mbili au tatu zijazo mtapitisha muswada wa kuanzisha divisheni ya mahakama ya mafisadi ili kupambana na watu wanaojihusisha na wizi na ufisadi,” alisema.
Alibainisha kuwa mahakama hiyo itadhibiti vitendo vya ufisadi na watakaojihusisha watachukuliwa hatua ili kuwa na watumishi wa umma wenye maadili mema.
Alisema watahakikisha Watanzania wanahudumiwa vizuri na watumishi waliopo waweze kutekeleza wajibu wao kwa Watanzania wote bila kuwa na vitendo vinavyoweza kuathiri utendaji wa kila siku.
Kuhusu uanzishaji wa somo la maadili kuanzia shule za msingi, Majaliwa alisema watakaa kuimarisha mabadiliko ya mitaala kwa kuingiza maeneo hayo ya utumishi bora na maadili mema.
No comments:
Post a Comment